AFCON U20 Q: Ngorongoro Heroes yaendelea na mazoezi
Kikosi cha timu Taifa ya Vijana chini ya umri wa miaka 20 'Ngorongoro Heroes' kimeendelea na mazoezi katika hosteli za Shirikisho la soka nchini (TFF) zilizopo Karume jijini Dar es Salaam kujiandaa na mchezo wa kuwania kufuzu kwenye fainali za Mataifa Afrika dhidi ya Congo DR.

Ngorongoro Heroes ambayo imeingia kambini toka Machi 8 mwaka huu ikiwa na kikosi cha wachezaji 43 tayari imepunguzwa kufikia wachezaji takribani 23 ambao wanaendelea na mazoezi.

Dhidi ya Morocco

Kikosi hicho kabla ya kuchuana na DR Congo mwishoni mwa mwezi huu, watakuwa na mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Morocco Jumamosi ya Machi 17 kwenye uwanja wa Taifa, Dar.

Kocha msaidizi wa Ngorongoro Heroes Oscar Mirambo ameutaja mchezo huo wa kirafiki kuwa kipimo tosha kabla ya kucheza na DR Congo.

"Mazoezi yanaendelea vizuri, kizuri ni kuwa wachezaji hawa tulikuwa nao mwaka jana wakiwa na Serengeti Boys na baadhi kutoka katika vilabu vyetu, tutacheza na Morocco mechi ya kirafiki ni jambo zuri kabla ya kucheza na DR Congo," Miramboa amesema.

Mshindi katika hatua hiyo atakutana na Mali katika hatua ya pili kuwania nafasi hiyo muhimu.

Kama Ngorongoro Heroes itafanikiwa kufuzu kwenye mashindano hayo itakuwa imejiwekea historia ya kushiriki Kwa mara ya kwanza kama ilivyokuwa kwa Michuano ya vijana chini ya umri wa miaka 17 Mwaka huu iliyofanyika Gabon.

Bingwa mtetezi

Bingwa mtetezi wa michuano hiyo ni Zambia ambaye alichukua taji Machi Mwaka jana, mashindano ambayo yalifanyika nchini Zambia.

Asilimia kubwa ya wachezaji wanaounda kikosi cha Ngorongoro Heroes ni wale ambao walishiriki michuano Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 iliyofanyika mwaka jana nchini Gabon