Billo: Waamuzi walikuwa upande wa Yanga
Kocha msaidizi wa timu ya soka ya  Stand United ya mjini Shinyanga, Athuman Bilal 'Billo Bilongo' amewatumia lawama waamuzi waliochezesha mchezo wao wa ligi kuu Tanzaania Bara dhidi ya Dar Young Africans kuwa ndio sababu ya wao kupoteza mchezo huo kwa mabao 3-1.

Billo amesema waamuzi hao walikuwa wakifanya maamuzi mengi ambayo yaliinufaisha Yanga kuliko kufuata kanuni zote 17 zinazotumika katika kuamua mchezo wa soka ulimwenguni kote.

"Asilimia kubwa tumepoteza mchezo kwa nguvu za mwamuzi, mwamuzi hakuwa sahihi kwa makosa madogo dogo ya hapa na pale, alitokea kuisaidia timu pinzani, kwa kweli waamuzi wa leo mimi binafsi sikuwafurahia," amesema Billo.

Akitoa mifano, Billo amesema bao la kwanza katika mchezo huo lilikuwa na utata kwani kabla ya Yussuf Mhilu kupokea mpira, mwamuzi msaidizi namba moja alinyanyua kibendera kuashiria offiside lakini mwamuzi wa kati akapeta.

"Hata goli la kwanza ukiangalia tumefungwa sio sahihi, kwa sababu mwamuzi msaidizi alinyoosha kibendera na wachezaji wangu walisimama, goli limeingia akashusha," aliongeza.

Wachezaji wake je?

Aidha Kocha huyo ambaye alishawahi kuzifundisha timu ya Toto Africans ya Mwanza, hakusita kuwalalamikia washambuliaji wake kwa kukosa umakini na kupoteza nafasi nyingi za wazi ambazo Stand United walitengeneza katika mchezo huo.

"Siwezi kuacha kuwalaumu wachezaji wangu kwa nafasi ambazo tulitengeneza na kupoteza, tumetengeza nafasi za wazi saba lakini tumepata bao moja, kwa hiyo washambuliaji hawakuwa makini, hilo tutalifanyia kazi," amesema.

Mchezo wa ligi baina ya timu hizo umefanyika katika Uwanja Taifa jijini Dar es Salaam Machi 12, 2018 huku mabao ya Yanga yakipatikana kupitia kwa Ibrahim Ajib, Obrey Chirwa na lile la kujifunga na Ally Ally huku bao pekee la Stand lilkifungwa na Vitali Mayanga.

Baada ya michezo 22 Stand United wamefanikiwa kukusanya alama 22, wakitoka sare michezo saba, wakifungwa michezo 10 na kushinda michezo mitano pekee, takwimu zinazowaweka katika nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi kuu soka Tanzania Bara, na tayari Billo amesema kuwa watajitahidi kuhakikisha wanapambana kusalia kwenye ligi hiyo inayoshirikisha jumla ya timu 16.