Yanga yawagawa mashabiki, waiunge mkono Simba au laaa!

Mabingwa wa soka wa kihistoria wa Tanzania Dar Young Africans, wameshindwa kuweka bayana kama wataishangilia Simba katika mchezo wao wa kombe la shirikisho dhidi ya Gendarmerie Nationale utakaofanyika Jumapili.

Kupitia kwa mkuu wa kitengo cha habari na mawasiliano Dismas Ten, klabu hiyo imesema wanawashukuru Simba kwa kusema wazi kuwa watawaunga mkono na kuwashangilia katika mchezo wao Jumamosi lakini wao muda wa kufanya hivyo bado haujafiki.

“Watanzania ni watu ambao tunahimizwa kudumisha amani tuliyonayo, hatuhitaji vita michezoni, hatuhitaji kutukanana, sisi tunawashukuru wale ambao wamejitokeza kwamba watatuunga mkono, hii ni nchi si jambo baya kufanya hivyo, wakati wa sisi kufanya hivyo ukifika na sisi tutasema” Dismas Ten.

Imefuta kauli ya Manara?

Ikumbukwe afisa habari wa Simba Haji Sunday Manara aliwaomba wanasimba wote kujitokeza kwa wingi na kufuta tofauti zao pale ambapo Yanga watakuwa dimbani kucheza na St Louis ya Shelisheli katika mchezo wa klabu Bingwa barani Afrika.

“Wanaliwakilisha taifa, kama hatuwezi kuwaunga mkono basi tusiwazomee,” alisema Manara.

Lakini kwa kauli ya Dismas Ten inawaweka njia panda mashabiki wa Yanga kama wanapaswa kuungana na wasimba siku ya Jumapili kwa kuishangilia ili kuweza kuibuka na ushindi.