Serikali: Hatujawazuia Yanga kufanya mazoezi Taifa, wafuate taratibu

Wasimamizi wa uwanja wa Taifa, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesema hawajawazuia timu ya Dar Young Africans kufanya mazoezi katika uwanja huo kama taarifa zinavyoeleza.

Akizungumza na mtandao huu mkurugenzi wa wizara ya Michezo Yusuph Omar Singo amesema kitu ambacho Yanga hawajakifanya ni kufuata utaratibu wa kuuomba uwanja huo kwa maandishi.

Singo amesema hana taarifa zozote mezani kwake za maombi ya Yanga kuutumia uwanja huo na kama angeiona basi asingekuwepo na sababu ya kuwakatalia kuutumia kwa mazoezi.

"Hayo maombi sijayaona mimi, labda nifuatilie kwa wasaidizi wangu lakini maombi yalipaswa kuja kwangu, uwanja hauwezi kuharibika ni kwamba taratibu tu zinatakiwa kufuatwa," amesema.

Hatupo nje kikanuni 

Kwa upande wake meneja wa uwanja wa Taifa Nsajigwa Gordon amesema wanachojaribu ni kuutunza uwanja huo hivyo mara zote wangependa kuona taratibu zinafuatwa katika matumizi yote yanayohusu uwanja huo.

Amesema hawapo nje kikanuni kwa Kuwazuia Yanga kufanya mazoezi hapo, kwani si lazima kwa mwenyeji kufanya mazoezi katika uwanja wake wa nyumbani kwani tayari anakuwa ameshauzoea.

Amesema wanachosubiri wao kwa sasa ni maombi kutoka kwa klabu ya Saint Louis ili kujua ni ratiba gani watawapangia katika kufanya mazoezi kabla ya mchezo siku ya Jumamosi.

"Huu sio uwanja wa mazoezi ni uwanja kwa ajili ya mechi, lakini kwa kuwa mgeni hajawahi kuutumia kanuni zinasema ni lazima wapate muda wa kufanya mazoezi kabla ya muda wa mechi," amesema Nsajigwa.

Saint Louis 

Yanga watacheza na Saint Louis katika mchezo muhimu wa hatua ya awali ya michuano ya klabu bingwa Barani Afrika Februari 10 mwaka huu katika uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam.

Kama Yanga watafanikiwa kufudhu katika hatua hiyo watakutana na Mshindi wa mchezo kati ya Township Rolers ya Botswana au Merrikh ya Sudan.