CAF CL: Yanga wazuiwa kufanya mazoezi uwanja wa Taifa

Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania Bara timu ya soka ya Dar Young Africans imenyimwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kuelekea katika mchezo wa hatua ya awali ya michuano ya klabu bingwa Barani Afrika.

Taarifa kutoka kwa viongozi wa benchi la timu hiyo wamesema kuwa walipofika asubuhi kwa ajili ya kufanya mazoezi walizuia kuingia uwanjani hivyo ikawabidi kwenda katika uwanja wa Polisi Bandali Kurasini kukamilisha utaratibu wao.

Katibu mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa amesema hawawezi kulazimisha kuutumia uwanja huo kwani inajulikana wazi kuwa wao ni wawakilishi wa kimataifa na serikali inatakiwa kuwapa kipaumbele.

"Sijazipata hizo taarifa rasmi ingawa tulikuwa tumefanya utaratibu wa kuomba, Unajua ni siku moja tu ambayo tuliwahi kuutumia kwenye ligi na hatujawahi kufanya mazoezi pale, na hatujapata majibu ya kama tumepata au hatujapata," ameeleza.

Uzalendo upo wapi? 

"Kama tumekosa hatuwezi kulazimisha sisi ni wawakilishi wa kimataifa na kama tunakosa kuutumia kwenye mazoezi basi ni taifa linalopotea, lazima tuwe na uzalendo Haya mashindano ni ya kwetu, tusipofanya vizuri tunalaumiwa," Mkwasa ameongoza.

Kanuni za kutumia uwanja ambao utatumika kwenye michuano ya kimataifa zipo wazi ambapo mwenyeji anapaswa kuutumia siku mbili na timu mgeni kutumia uwanja huo siku moja kabla ya mchezo.

Ikumbukwe Yanga watajitupa uwanjani Jumamosi ya Februari 10 kucheza na Saint Louis ya Shelisheli katika uwanja wa Taifa kwenye michuano ya awali ya klabu Bingwa Afrika.