CAF CL: Zesco United wawasili salama visiwani Zanzibar

Wapinzani wa timu ya soka ya JKU ya Zanzibar katika michuano ya klabu bingwa Afrika timu ya Zesco United kutoka Zambia wamewasili Jumatano ya Februari 7 Visiwani Zanzibar tayari kabisa kwa mchezo wa Jumamosi kwenye uwanja wa Amaan.

Timu hiyo imewasili majira ya saa nne asubuhi kwenye uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume kwa ndege ya Shirika la Kenya ambapo wachezaji wa timu hiyo wameongozana na viongozi wao na wamepokelewa na wenyeji wao ambao ni viongozi wa timu ya JKU na chama cha soka Zanzibar ‘ZFA’.

Afisa habari wa chama cha soka Zanzibar (ZFA) Ali Bakar (Cheupe) amesema kwa upande wao kama Chama, maandalizi yote wamekamilisha huku akiwataka Mashabiki wa soka kujitokeza kwa wingi kwenda kuzishangilia timu za Zanzibar.

“ZFA tushajiandaa kwa ajili ya michezo yote ya kimataifa ambayo itapigwa hapa mwishoni mwa juma,tuna timu za Zimamoto na JKU, kwa kifupi maandalizi yamekamilika ikwemo hoteli kwa ajili ya wageni wetu na uwanja kwa ujumla wake,” amesema Cheupe.

Wachezaji waliofika

Wachezaji waliowasili ni pamoja na walinda milango Jacob Banda na Dieudonne Ntibahezwa, huku mabeki wakiwa ni Solomon Sakala, Fackson Kapumbu, Marcel Kalonda, Simon Silwimba, Daut Musekwa na David Owino.

Viungo ni Akumu Anthony Agay, Kondwani Mtonga, John Chinga’ndu, Mwape Mwelwa, Enoch Sabumukama na Lameck Banda, wakati washambuliaji wakiwa ni pamoja na  Jackson Mwanza, Lazarus Kambole, Jesse Were na Winston Kalengo.

Wawakilishi wa Zanzibar katika Mashindano hayo ya Kimataifa ni JKU ambao wataivaa Zesco United siku ya Jumamosi katika mchezo wa kombe la Klabu bingwa huku Zimamoto ambao watawakilisha kwenye kombe la Shirikisho wataivaa Walaitta Dicha ya Ethiopia siku ya Jumapili michezo yote itapigwa majira ya saa 10:00 za jioni katika uwanja wa Amaan mjini Unguja.